Genesis 48:5-16

5 a“Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa ni wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu. 6Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao. 7 bNilipokuwa ninarudi kutoka Padani, katika huzuni yangu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tungali tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrathi. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrathi” (yaani Bethlehemu).

8 cWakati Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akauliza, “Hawa ni nani?”

9 dYosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.”

Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.”

10 eBasi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yosefu akawaleta wanawe karibu na baba yake, Israeli akawabusu na akawakumbatia.

11 fIsraeli akamwambia Yosefu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.”

12Ndipo Yosefu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli naye akasujudu hadi nchi. 13 gYosefu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao. 14Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa ndiye mdogo, na mkono wake wa kushoto akaukatisha, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase alikuwa ndiye mzaliwa wa kwanza.

15Ndipo akambariki Yosefu akisema,

“Mungu ambaye baba zangu
Abrahamu na Isaki walimtii,
Mungu ambaye amekuwa mchungaji
wa maisha yangu yote mpaka leo hii,
16 hMalaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote,
yeye na awabariki vijana hawa.
Na waitwe kwa jina langu
na kwa majina ya baba zangu Abrahamu na Isaki,
wao na waongezeke kwa wingi
katika dunia.”
Copyright information for SwhNEN